.

.

MUNA TOYS & STATIONERY

MUNA TOYS & STATIONERY

Friday, May 16, 2014

KAMA ULIKUWA NA MPANGO WA KUKATA TAMAA, SOMA HII ITAKUSAIDIA?



              
Bwana mmoja alikuwa anaitwa KAKABRAZA, alikuwa amefungwa kwenye mahabusu chafu sana,akiwa humo ndani alimwona mdudu mdogo sana ambaye husukuma mzigo wake kwa miguu, akatulia kidogo kumwangalia akijaribu kupandisha mzigo mkubwa kuliko yeye kwenye ukuta mrefu! Akavutiwa kidogo na tukio hilo, akitaka kujua nini hasa ilikuwa lengo la mdudu huyo na kama kweli angeweza kupandisha mzigo mkubwa kiasi hicho katika ukuta mrefu .



Ukuta ulikuwa kama wa mita sita hivi, basi akamshuhudia mdudu kwa mara ya kwanza akisukuma mzigo wake kwa miguu  sentimita kama mia moja hivi akaporomoka nao  moja kwa moja hadi chini! Tofauti na alivyofikiria KAKABRAZA kuwa kwa jinsi alivyoporomoka mdudu huyo asingethubutu tena kujaribu kupandisha mzigo unao mzidi uwezo katika ukuta huo, alishangaa  kumwona mdudu anaanza tena safari ya kupandisha mzigo ule ule, safari hii alikwenda kama sentimita mia mbili na hamsini hivi, akaporomoka tena mpaka chini! Akamuhurumia na kuamini kuwa huo ndio ulikuwa ndio mwisho wake

Haukupita muda mrefu,akashangaa kumwona mdudu anaukamata tena mzigo wake kwa miguu na kuanza kuusukuma taratibu, safari hii alikwenda kama sentimita mia nne  kabla ya kuporomoka tena hadi chini!  KAKABRAZA  akashika kichwa kwa masikitiko makubwa sana akimwonea huruma, tayari suala hilo lilishamwingia sana moyoni KAKABRAZA na kuteka hisia zake. Akiendelea kutafakari nini kingefuata, alimwona mdudu anaukamata tena mzigo wake kuanza  safari  ya kupandisha ukuta, safari hii akavuka sentimita mia nne na kukaribia hadi sentimita mia saba na kuporomoka tena chini,

Kila alipoporomoka mdudu huyo  alikwenda moja kwa moja hadi chini na kuanza upya lakini safari hii alizidi alipokomea mwanzo, bila shaka kuna kitu alijifunza na kurekebisha ndiyo maana akaenda sentimita nyingi zaidi juu!  Alifanya hivyo kwa kutokukata tamaa hatimaye akafanikiwa kumaliza mita zote sita na kupotelea darini, KAKA BRAZA alishindwa kuvumilia akanyanyuka chini alipokuwa ameketi na kushangilia kama vile goli limefungwa akitamka maneno haya” KAMWE MWANADAMU HUTAKIWI KUKATA TAMAA NA NI LAZIMA UJIWEKEE LENGO KUBWA MAISHANI MWAKO”

Kama mdudu anaweza kufanya hivi inakuwaje mwanadamu ashindwe? Mdudu alikuwa na lengo la kuvuka ukuta, akaanguka mara kadhaa lakini hakukata tamaa, alijifunza kutokana na makosa ya nyuma na kuendelea na safari yake hatimaye akafanikiwa!  Hivi ndivyo wanadamu tunavyotakiwa kufanya katika maisha yetu ya kila siku, lazima tujiwekee malengo, haiwezekani hata kidogo kuishi bila ya malengo na kutokuelewa unataka nini, lini na kwanini?

3 comments:

 

Bongo Blogs - Blog ya Taifa

COPYRIGHT © Egy business solution DESIGN BY NANG JET 0764504595,0672804085